Timu ya Simba ilifanya maajabu ya kuingia katika kitabu cha Guiness na kuweka rekodi barani Afrika kwa kuifunga Mufurila Wanderers ya Zambia magoli 5-0 nyumbani kwao.
Simba katika mchezo wa awali uliofanyika kwenye uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam ilifungwa magoli 4-0 na Mufurila, hivyo kwenda Zambia ikiwa na matumaini finyu ya kupata ushindi. Mashabiki wengi walipendekeza timu hiyo isiende Zambia kwa hofu ya kipigo cha magoli mengi zaidi.
Simba ilikwenda Zambia kwa kutumia njia ya treni na katika pambano hilo la marudiano mgeni wa heshima alikuwa, Rais Kenneth Kaunda wa Zambia.
Magoli ya Simba yalifungwa na George Kulagwa dakika ya 12, Thuwein Ally dakika ya 19 na Abdallah Mwinyimkuu dakika ya 34. na hadi timu zinakwenda mapumziko Simba ilikuwa ikiongoza kwa mabao 3-0.
Kipindi cha pili Abbas Dilunga aliipatia Simba goli la nne dakika ya 59 na dakika ya 72 Abdallah Mwinyimkuu aliipatia Simba goli la tano .
Baada ya mchezo watanzania ambao walikuwa wakiishi Zambia waliamka vitini na kushangilia kwa nguvu zao zote. Mbali ya kushangilia huko Watanzania hao waliandaa pati iliyofanyika katika bar ya Mtanzania mwenzao Eddy Sally.
Kikosi cha Simba kilifundishwa na jopo la makocha akiwemo Joel Bendera ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro.
Kikosi cha simba kilipangwa hivi: Athumani Mambosasa, Daudi Salum, Mohamed Kajole, Philbert Rubibira, Hussein Tindwa, Abbas Kuka, George Kulagwa, Abdallah Mwinyimkuu, Thuwein Ally, Ismail Mwarabu, Abbas Dilunga/Abdallah Hussein.