Wachezaji mahiri wa timu ya Simba kiungo Athumani Juma na mshambuliaji Adam Sabu walijiunga na mahasimu wa jadi Yanga.
Athumani Juma aliyekuwa na uwezo mkubwa wakumiliki mpira na kupiga mashuti ya nguvu na Sabu mshambuliaji mwenye nguvu na uwezo wa kufunga magoli, walikaa katika Yanga kwa muda wa wiki mbili.
Wachezaji hao walirejea katika timu yao ya Simba baada ya kutakiwa na wachezaji wenzao wakati wa safari ya mechi kwenda Tabora.
Wakiwa katika stesheni ya reli jijini Dar es Salaam, wachezaji walimwomba Meneja wao kutaka kuongozana na wenzao.
Meneja huyo aliwafuata majumbani kwao na kuwaeleza kuwa wanaitwa na wenzao kwa ajili ya kurejea Simba na kwenda katika ziara ya Tabora. Wachezaji hao ambao kwa sasa ni marehemu walikubali ombi hilo na kuchukua mabegi yao kuelekea stesheni kwa ajili ya safari ya Tabora.